Add parallel Print Page Options

Yesu Afariki

(Mk 15:33-41; Lk 23:44-49; Yh 19:28-30)

45 Ilipofika adhuhuri, giza liliifunika Israeli yote kwa muda wa masaa matatu. 46 Yapata saa tisa alasiri Yesu alilia kwa sauti kuu akisema, “Eloi, Eloi, lema sabakthani?” yaani “Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniacha peke yangu?”(A)

47 Baadhi ya watu waliosimama pale waliposikia hili wakasema, “Anamwita Eliya.”[a]

48 Mtu mmoja alikimbia haraka akaenda kuchukua sponji, akaijaza siki, akaifunga kwenye fimbo na akanyoosha fimbo ili kumpa Yesu sponji ili anywe siki. 49 Lakini wengine walisema, “Usimjali. Tunataka tuone ikiwa Eliya atakuja kumsaidia.”

50 Yesu akalia kwa sauti kuu tena, kisha akafa.[b]

51 Yesu alipokufa, pazia la Hekalu lilipasuka vipande viwili. Mpasuko wake ulianzia juu mpaka chini. Kulitokea pia tetemeko la ardhi na miamba ilipasuka. 52 Makaburi yalifunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa walifufuka kutoka kwa wafu. 53 Walitoka makaburini. Na baada ya Yesu kufufuliwa kutoka kwa wafu, walikwenda kwenye mji mtakatifu wa Yerusalemu, na watu wengi waliwaona.

54 Afisa wa jeshi na askari waliokuwa wanamlinda Yesu walitetemeka sana kwa kuogopa tetemeko la ardhi na kila walichokiona kikitokea. Wakasema, “Hakika alikuwa Mwana wa Mungu!”

55 Wanawake wengi waliomfuata Yesu kutoka Galilaya kumhudumia walikuwepo pale wakiangalia wakiwa wamesimama mbali na msalaba. 56 Miongoni mwao alikuwepo Mariamu Magdalena, Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu na pia mama yao Yakobo na Yohana[c] alikuwepo pale.

Read full chapter

Footnotes

  1. 27:47 Anamwita Eliya Neno hili “Mungu wangu” (ni Eli kwa Kiebrania ama Eloi kwa Kiaramu) ilisikika kwa watu kama jina la Eliya. Nabii maarufu aliyeishi mikaka kama 850 KK.
  2. 27:50 akafa Kwa maana ya kawaida, “roho yake ikamwacha”.
  3. 27:56 Yakobo na Yohana Kwa maana ya kawaida, “wana wa Zebedayo”.