Add parallel Print Page Options

Yohana alipokuwa gerezani, alisikia kuhusu mambo yaliyokuwa yanatokea; mambo ambayo Masihi angefanya. Hivyo akawatuma baadhi ya wafuasi wake kwa Yesu. Wakamuuliza, “Wewe ni yule tuliyekuwa tunamngojea, au tumsubiri mwingine?”

Yesu akajibu, “Rudini mkamwambie Yohana yale mliyosikia na kuona: Vipofu wanaona. Viwete wanatembea. Watu wenye magonjwa ya ngozi wanaponywa. Wasiyesikia wanasikia. Wafu wanafufuliwa. Na habari njema inahubiriwa kwa maskini. Heri ni kwa wale wasio na shida kunikubali.”

Wafuasi wa Yohana walipoondoka, Yesu alianza kuongea na watu kuhusu Yohana. Alisema, “Ninyi watu mlikwenda jangwani kuona nini? Mtu aliye dhaifu, kama unyasi unaoyumbishwa na upepo? Hakika, ni nini mlichotarajia kuona? Aliyevaa mavazi mazuri? Hakika si hivyo. Watu wote wanaovaa mavazi mazuri wanapatikana katika ikulu za wafalme. Hivyo mlitoka kuona nini? Nabii? Ndiyo, Yohana ni nabii. Lakini ninawaambia, Yeye ni zaidi ya hilo. 10 Andiko hili liliandikwa kuhusu Yohana:

‘Sikiliza! Nitamtuma mjumbe mbele yako.
    Yeye ataandaa njia kwa ajili yako.’(A)

11 Ukweli ni kuwa Yohana Mbatizaji ni mkuu kuliko yeyote aliyewahi kuja katika ulimwengu huu. Lakini hata mtu asiye wa muhimu katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko Yohana. 12 Tangu wakati wa Yohana Mbatizaji ulipokuja mpaka sasa, Ufalme wa Mungu umekabiliwa na mashambulizi. Watu wenye nguvu wamejaribu kuudhibiti ufalme huu.[a] 13 Kabla ya Yohana kuja, Sheria ya Musa na manabii wote wamesema kuhusu mambo ambayo yangetokea. 14 Na ikiwa mnaamini waliyosema, basi Yohana ni Eliya. Ndiye waliyesema angekuja. 15 Ninyi watu mnaonisikia, sikilizeni!

16 Ninaweza kusema nini kuhusu watu wanaoishi leo? Watu siku ya leo ni kama watoto wanaokaa katika masoko. Kundi moja la watoto linaliambia kundi lingine,

17 ‘Tuliwapigia filimbi,
    lakini hamkucheza;
tuliimba wimbo wa maziko,
    lakini hamkuhuzunika.’

18 Kwa nini ninasema watu wako hivyo? Kwa sababu Yohana alikuja na hakula vyakula vya kawaida na kunywa divai, na watu walisema, ‘Ana pepo ndani yake.’ 19 Mwana wa Adamu amekuja akila na kunywa, na watu husema, ‘Mwangalie! Hula sana na kunywa divai nyingi. Ni rafiki wa wakusanya kodi na wenye dhambi wengine.’ Lakini hekima inaonesha kuwa sahihi kutokana na yale inayotenda.”

Read full chapter

Footnotes

  1. 11:12 Herode Antipa alimkamata na kisha kumwua Yohana Mbatizaji na pia alijaribu kumzuia Yesu na wanafunzi wake kwa nguvu. Tazama Herode katika Orodha ya Maneno.