Add parallel Print Page Options

Yesu Akiwa Mbele ya Viongozi wa Kidini

(Mt 26:57-68; Lk 22:54-55,63-71; Yh 18:13-14,19-24)

53 Nao wakamwongoza Yesu kumpeleka kwa kuhani mkuu, na viongozi wote wa makuhani, wazee, na walimu wa Sheria walikutanika. 54 Petro akamfuata Yesu kwa mbali kidogo hadi ndani ya baraza la nyumba ya kuhani mkuu. Petro alikuwa ameketi na wale walinzi akijipasha joto na moto walioukoka.

55 Viongozi wa makuhani na Baraza lote la Wayahudi walikuwa wakitafuta ushahidi dhidi ya Yesu wa kuweza kumhukumu kifo, lakini hawakupata kitu chochote. 56 Watu wengi walikuja na kutoa ushahidi wa uongo dhidi yake, lakini wote walisema vitu tofauti. Ushahidi wao ulipingana.

57 Kisha wengine walisimama na kushuhudia kinyume chake kwa uongo, wakisema, 58 “Tulimsikia mtu huyu[a] akisema, ‘Nitaliharibu Hekalu hili lililotengenezwa kwa mikono ya wanadamu, na kwa siku tatu nitajenga lingine ambalo halikujengwa kwa mikono.’” 59 Lakini hata katika ushahidi wao huu hawakukubaliana.

60 Kisha kuhani mkuu akasimama mbele yao na akamwuliza Yesu, “Je, wewe hutajibu? Nini ushahidi huu ambao watu wanaleta dhidi yako?” 61 Lakini Yesu alinyamaza kimya na hakutoa jibu lolote.

Kwa mara nyingine kuhani mkuu akamwuliza, “Je, wewe ni Kristo, Mwana wa Mungu anayesifiwa?”

62 Yesu akasema, “Mimi ndiye. Nanyi mtamwona Mwana wa Adamu akiketi mkono wa kuume wa Mungu Mwenye uweza wote akija pamoja na mawingu ya mbinguni.”[b]

63 Kuhani mkuu alichana mavazi yake na kusema, “Tuna haja gani ya kuleta mashahidi zaidi? 64 Ninyi wote mmesikia akimtolea Mungu matusi.”

Wote walimhukumu na kumwona kwa anastahili kifo. 65 Na wengine walianza kutema mate, na kufunika uso wake, na kumpiga, na kumwambia, “Uwe nabii na utuambie nani aliyekupiga.” Kisha wale walinzi walimchukua na kuendelea kumpiga.

Read full chapter

Footnotes

  1. 14:58 mtu huyu Yaani, Yesu. Adui zake walikuwa wanakwepa kutamka jina lake.
  2. 14:62 Mwana wa Adamu … ya mbinguni Tazama Dan 7:13 na Zab 110:1.